JAY RUTTY AMWAGA MABILIONI SIMBA SC

ZILIZO KIKI (BONGO) 🚨

Wakati mkataba wa miaka miwili wa Kampuni ya Sandaland kuhusu uzalishaji wa vifaa vya michezo kwa Club ya Simba SC ukiwa unaelekea ukingoni, Club hiyo jioni ya leo Jijini Dar es salaam imemtangaza Mzalishaji mpya wa jezi zao.

Simba wamemitangaza Kampuni ya Jayrutty kuwa ndio Mzalishaji na Muuzaji mpya wa jezi zao kwa kipindi cha miaka mitano katika mkataba huo mnono wenye thamani ya Tsh Bilioni 38 (38,120,400,000).

Kwa mujibu wa mkataba, licha ya Kampuni hiyo kutengeneza jezi za Timu huyo pia itajenga uwanja wa Simba SC wenye uwezo wa kuchukua mashabiki kati ya elfu 10 hadi 12, kuleta basi jipya la kisasa la Timu aina ya Irizar, kujenga Media ya Club, Ofisi na kutoa pesa Tsh milioni 100 kila mwaka za kusaidia vipaji vya soka vya Simba SC.

Mkataba huu mpya unakuwa mkataba ulioweka rekodi ya kipekee kwa Tanzania na Afrika Mashariki kwani imeelezwa kuwa hakuna Club yoyote ya soka yenye mkataba wa thamani hiyo.

Mwaka 2019 Simba iliingia mkataba wa miaka miwili na UhlSport wenye thamani ya Tsh milioni 600, mwaka 2021 wakasaini mkataba wa miaka miwili na Vunjabei wenye thamani ya Tsh Bilioni 2 na mwaka 2023 waliingia Mkataba wa miaka miwili na Sandaland wenye thamani ya Tsh Bilioni 4.